1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Rais wa Kenya Ruto asaini mswada wa fedha 2023

Thelma Mwadzaya26 Juni 2023

Wakenya wanajiandaa kwa kipindi kigumu baada ya mswada wa fedha wa 2023 kutiwa saini kuwa sheria. Sheria hiyo mpya itaongeza pato la serikali kupitia nyongeza ya kodi kufadhili bajeti mpya ya shilingi trilioni 3.6

https://p.dw.com/p/4T43W
Kenias Präsident William Ruto
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Akiwa kwenye ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto alitia saini mswada wa fedha wa 2023 kuwa sheria. Sheria hii mpya ilizua mjadala mkali bungeni wiki iliyopita wakati viongozi 88 wa upinzani walipoupinga ila walishindwa nguvu na wale wanaoegemea serikali wa Kenya Kwanza walioupitisha kwa kura 184.

Soma pia:Polisi Kenya watawanya maandamno dhidi ya mswada wa fedha

Kwa mantiki hii, Wakenya watalazimika kulipa kodi zaidi kufadhili bajeti ya kwanza ya Rais William Ruto ya shilingi trillion 3.6. Serikali inasema bajeti hiyo ina azma ya kumuinua kiuchumi Mkenya wa tabaka la chini . Rais William Ruto anasisitiza kuwa Kenya si ya mtu mmoja.

Kodi mpya zilizopitishwa kwenye sheria mpya ya fedha ni ya mafuta ya petroli kutokea 8 % hadi 16%, ya makaazi mapya iliyopunguzwa kutokea 3% hadi 1.5% ya mshahara Kamili, hali inayozua mitazamo tofauti. Wanaosambaza vipindi kupitia mitandao sasa watatozwa kodi ya 5% iliyopunguzwa kutokea 15%. Kimani Ichungwah ni kiongozi wa Chama tawala bungeni na huu ndio mtazamo wake.

Kenia Kenianische Aktivisten demonstrieren in Nairobi gegen ein unpopuläres Finanzgesetz
Mswada huo ulikabiliwa na upinzani mkaliPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Hata hivyo, sheria hiyo mpya huenda ikaandamwa na vikwazo vipya. Chama cha wanasheria nchini Kenya, LSK, kinajiandaa kufika mahakamani kupinga ukusanyaji wa kodi hizo mpya ambao umepangwa kuanzia Julai mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa LSK, Eric Theuri, wanasheria watawasilisha kesi mahakamani hii leo au kesho kupinga utekelezaji wa kodi hizo mpya. Wakati huohuo, wanasiasa wa upinzani wanafanya mhadhara kesho Jumanne kwenye uwanja wa Kamukunji kupanga mbinu za kuishinikiza serikali kufutilia mbali hatua hizo mpya. Opiyo Wandayi ni kiongozi wa upinzani bungeni na anasisitiza kuwa umma ndio utakaoamua.

Katibu mkuu wa Chama cha UDA cha rais William Ruto Cleophas Malala alikuwa na haya ya kusema kuhusu maandamano ya kesho.

Kwa upande mwengine, wafanyakazi wa umma nao pia wametishia kugoma kupinga nyongeza ya kodi. Kulingana na katibu mkuu wa muungano wa wafanyakazi wa vyuo vikuu, Constantine Wasonga, wako tayari kwenda mahakamani kadhalika wanatathmini uwezekano wa kuandaa mgomo.

Yote hayo yakiendelea, wabunge waliridhia mageuzi kwenye sheria ya kustaafu ili kuwanufaisha baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu. Kwenye mabadiliko hayo, raisi, waziri kiongozi, spika wa bunge na senate wa sasa na awali watapokea malipo ya uzeeni kuzingatia nafasi walizoshikilia awali na mshahara wa nyadhifa wanazohudumu kwa sasa pamoja na Kitita maalum cha malipo ya mpigo.