1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto amhamisha waziri wa mambo ya nje Alfred Mutua

Iddi Ssessanga
5 Oktoba 2023

Rais wa Kenya William Ruto amefanya mabadiliko ya kwanza katika baraza lake la mawaziri ambamo amewaondoa washirika wake kutoka nyadhifa kuu katikati mwa kutoridhika kutokana na kukiuka ahadi na matatizo ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/4XAaQ
Kenya I Rais William Ruto
Rais William Ruto amefanya mabadiliko baada ya kuwashtumu baadhi ya mawaziri wake kwa utendaji mbovu.Picha: Tony Karumba/AFP

Rais wa Kenya William Ruto amefanya mabadiliko ya kwanza katika baraza lake la mawaziri katika mabadiliko yaliyowaondoa washirika wake kutoka nyadhifa kuu huku kukiwa na hali ya kutoridhika kutokana na kukiuka ahadi na matatizo ya kiuchumi.

Waziri wa Mambo ya Nje Alfred Mutua, ambaye amekuwa mtetezi mkubwa wa Kenya kutuma polisi katika ujumbe wa kulinda amani nchini Haiti iliyokumbwa na ghasia, amehamasishiwa wizara ya utalii.

Katika nafasi yake, Waziri Kiongozi Musalia Mudavadi aliona wadhifa wake ukipanuliwa na kujumuisha masuala ya kigeni.

Mabadiliko hayo - yaliofanyika wiki chache baada ya Ruto kuwashutumu baadhi ya mawaziri wake kwa kutokuwa na uwezo -- yalikusudiwa "kuboresha utendakazi na utoaji wa huduma," ofisi ya Ruto ilisema katika taarifa Jumatano.

Marekani I Kenya I  Alfred Mutua na  Antony Blinken
Waziri wa zamani wa mambo ya nje Alfred Mutua akiwa na mwenzake wa Marekani Antony Blinken mjini Washington, Aprili 24, 2023. Mutua sasa amehamishwa kutoka wizara ya mambo ya nje.Picha: Carolyn Kaster/AP/picture alliance

Soma pia: Rais wa Kenya afanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri

Waziri wa Biashara Moses Kuria, mbunge wa zamani ambaye ameibua mabishano kuhusu matamshi kadhaa ya kashfa, alikabidhiwa wizara ya utumishi wa umma.

Mnamo Juni, Kuria alisababisha dhoruba alipozua kizaazaa dhidi ya chombo kikuu cha habari na kutishia maafisa wa serikali waliotangaza na chombo hicho kuwafuta kazi.

Kuria alipuuzwa na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Katherine Tai alipozuru Nairobi mnamo Julai na hakuwepo wakati wa ziara mbili za mwisho za rais mjini Washington.

Soma pia: Marekani na Kenya zasaini makubaliano ya ulinzi

Nafasi ya Kuria itachukuliwa na Rebecca Miano ambaye alikuwa anasimamia uhusiano wa kikanda na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kiprotich arap Cherargei, seneta kutoka chama tawala na mshirika wa karibu wa Ruto, alisema mabadiliko hayo "yamechochewa na haja ya kuboresha na utendaji kazi".

Onyo kwa watendaji wabovu

"Maandishi yapo ukutani kwa mawaziri wasiofanya kazi na wale wanaoendeleza ufisadi na uzembe katika wizara zao," alichapisha kwenye mtandao wa X, zamani Twitter.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana, Ruto alijitanabahisha kama mtetezi wa maskini lakini amekuwa akishutumiwa pakubwa kwa kuvunja ahadi.

Je, maandamano ndio suluhu ya matatizo yanayoizonga nchi?

Wiki hii aliagiza wizara kupunguza matumizi kwa asilimia 10 na akapunguza usafiri wa nje kwa maafisa wa serikali, huku deni la umma likipanda hadi dola bilioni 68.9.

Wakenya tayari wanakabiliwa na kupanda kwa bei ya bidhaa nyingi kuu, msururu wa ushuru mpya au ulioongezeka na shilingi inayoshuka.

Gharama ya mafuta nchini Kenya ilipanda kwa viwango vya juu kabisaa mwezi uliopita huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa serikali inazingatia nyongeza zaidi ya ushuru, ikiwa ni pamoja na kuongeza VAT na ushuru unaolenga wakulima na wamiliki wa magari.

Msururu wa maandamano ya upinzani dhidi ya serikali ya Ruto na sera zake za kiuchumi ulifanyika mwaka huu, baadhi yakigeuka kuwa ghasia mbaya.