1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la UN kuhusu mauaji ya Srebrenica lazusha upinzani

Tatu Karema
17 Mei 2024

Azimio la Umoja wa Mataifa lililowasilishwa na Ujerumani na Rwanda la kuanzisha maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya waislamu zaidi ya 8,000 wa Bosnia yaliyofanywa na Waserbia limezusha upinzani.

https://p.dw.com/p/4fyft
Ndugu za jamaa wa mauaji ya Srebrenica
Ndugu za jamaa wa mauaji ya Srebrenica Picha: Klix.ba

Azimio la Umoja wa Mataifa lililowasilishwa na Ujerumani pamoja na Rwanda la kuanzisha maadhimisho ya kila mwaka ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya waislamu zaidi ya 8,000 wa Bosnia ya mwaka 1995 yaliyofanywa na Waserbia wa Bosnia, limezua tuhuma kali na kampeini dhidi ya kuidhinishwa kwake kutoka kwa Rais wa Serbia na uongozi wa Waserbia wa Bosnia.

Soma: Uholanzi yaiomba radhi Srebrenica kwa mauaji

Katika taarifa, balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa Antje Leendertse, amesema kuna siku maalumu ya Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ambayo ni Aprili 7 kila mwaka na kwamba azimio hilo linalenga kuziba pengo kwa kuanzisha siku tofauti ya Umoja huo ya kuwakumbuka wahanga hao wa Bosnia kwa wakati kabla ya maadhimisho ya miaka 30 ya mauaji hayo mnamo mwaka 2025.

Miaka 25: Wabosnia waadhimisha miaka 25 ya mauaji ya Srebrenica

Rais wa Serbia Aleksandar Vucic pamoja na uongozi wa Waserbia nchini Bosnia, wamepinga vikali kuidhinishwa kwa azimio hilo na kusema linawataja Waserbia wote kama "taifa la mauaji ya halaiki'' ijapokuwa rasimu ya azimio hilo  haijawataja Waserbia kama wakosaji.