1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yamshutumu mkuu wa WHO kwa kuwasaidia waasi

Grace Kabogo
19 Novemba 2020

Mkuu wa majeshi ya shirikisho ya Ethiopia amemshutumu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwa kuwasaidia waasi wa jimbo la Tigray kupata silaha.

https://p.dw.com/p/3lXgL
Äthiopien General Berhanu Jula PK
Picha: DW/S. Muchie

Akizungumza na waandishi habari, Jenerali Berhanu Jula amesema Tedros anaungana na nchi jirani kulaani vita, lakini anashirikiana na waasi kwa kuwapatia silaha.

Berhanu amesema kiongozi huyo wa WHO pia anatoa msaada wa kidiplomasia kwa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, ambacho Waziri Mkuu Abiy Ahmed anasema anakilenga katika mashambulizi ya kijeshi kwenye jimbo hilo la kaskazini.

Berhanu amebainisha kwamba Tedros ambaye anatoka jimbo la Tigray na aliyewahi kuwa waziri wa afya wa Ethiopia katika serikali iliyopita ni sehemu ya waasi wa Tigray, hivyo hawetegemei awe upande wa watu wa Ethiopia na kulaani kinachofanywa na vikosi vya TPLF. ''Huyu mwenyewe ni sehemu ya timu ya waasi, na kama unavyojua yeye ni sehemu ya kamati kuu ya chama cha TPLF,'' alifafanua Berhanu.

Schweiz Genf WHO Treffen | Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: picture-alliance/Xinhua/WHO

Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha TPLF, Debretsion Gebremichael, amesema mji wa Axum bado uko mikononi mwao, ingawa mji mwingine wa Shire unadhibitiwa na majeshi ya serikali, ambayo yanakaribia kuingia kwenye mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekele.

Debretsion amesema siku tatu zilizopita mji wa Shire uliangukia mikononi mwa majeshi ya serikali, ingawa vikosi vyake bado vinaudhibiti mji wa Axum. Hata hivyo, mkuu wa kikosi kazi cha serikali ya Ethiopia kinachohusika na mashambulizi ya Tigray hajazungumzia taarifa hizo.

Waasi wafanya ukatili mkubwa

Ama kwa upande mwingine serikali ya Ethiopia imesema waasi wa Tigray wamefanya ukatili na uhalifu mkubwa katika mapigano ya wiki mbili. Mzozo huo umewaua mamia ya Waethiopia, huku watu wengine 30,000 wakilazimika kukimbilia nchi jirani ya Sudan. Taarifa hiyo ya serikali inarejelea ripoti ya mauaji ya kikabila kwenye mji wa Mai Kadra, yaliyoorodheshwa wiki hii na shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International.

Äthiopien l PK - Dr. Debretsion Gebremichael
Picha: DW/M. Haileselassie

Watu walionusurika na mashambulizi hayo wamewaambia watafiti wa Amnesty International kwamba waasi wanaofungamana na serikali ya jimbo la Tigray waliwaua mamia ya raia, baadhi yao wakiwa wa kabila la Amhara.

Hata hivyo, imekuwa vigumu kuzithibitisha taarifa hizo kutoka pande zote, kwa sababu huduma za intaneti na simu kwenye jimbo hilo zimekatwa na serikali imewazuia watu kuingia katika eneo hilo.

Aidha, mshauri wa rais mteule wa Marekani, Joe Biden anayehusika na sera ya kigeni, Antony Blinken ametoa wito wa raia kulindwa kwa kiasi kikubwa.

Blinken amesema wana wasiwasi mkubwa kuhusu mzozo wa kibinaadamu nchini Ethiopia, taarifa za kuzuka mzozo wa kikabila na hatari ya kuvurugika kwa usalama na amani kwenye kanda hiyo. Amesema chama cha TPLF na viongozi wa Ethiopia wanapaswa kuchukua hatua za haraka kuumaliza mzozo huo, kusaidia kupatikana kwa msaada wa kibinaadamu na kuwalinda raia.

(AFP, Reuters)