1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya awali yakipa ushindi SPD Saarland

Grace Kabogo
28 Machi 2022

Chama cha Social Democratic, SPD kimetangazwa mshindi katika uchaguzi wa jimbo la magharibi mwa Ujerumani, Saarland.

https://p.dw.com/p/4971M
Plakate zur Landtagswahl im Saarland | Tobias Hans CDU und Anke Rehlinger SPD
Picha: BeckerBredel/IMAGO

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na vituo vya utangazaji vya umma ARD na ZDF, chama hicho cha Kansela Olaf Scholz kimeshinda uchaguzi wa jimbo hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20, kwa kupata asilimia 43.5 ya kura.

Matokeo ya awali yaliyotolewa na bodi ya uchaguzi ya serikali yanaonesha kuwa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU kimepata asilimia 28.5 ya kura na hivyo kuwa matokeo mabaya zaidi katika kipindi cha miaka 67.

Uchaguzi wa Jumapili ni wa kwanza kufanyika Ujerumani tangu serikali ya shirikisho ya Kansela Scholz ilipoingia madarakani mwezi Desemba, mwaka uliopita. 

Deutschland Saarbrücken | Landtagswahl | Wahlsiegerin Anke Rehlinger
Anke Rehlinger wa SPD anayetarajiwa kuwa waziri mkuu mpya wa jimbo la SaarlandPicha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Tangu mwaka 1999 jimbo la Saarland limekuwa likiongozwa na Angela Merkel. Katika uchaguzi huo wa jana, SPD ilipata viti 29 kati ya 51, hivyo kuwa na wingi wa kura. Hatua hii inamaanisha kuwa SPD hawatolazimika kuunda serikali ya muungano. SPD kimeongeza kura kwa takribani asilimia 14 kutoka katika uchaguzi wa mwisho uliofanyika miaka mitano iliyopita, huku CDU ikiporomoka kwa asilimia 12.

Anke Rehlinger kuwa waziri mkuu mpya

Kutokana na matokeo hayo Anke Rehlinger wa SPD, sasa atakuwa waziri mkuu mpya wa jimbo la Saarland, akichukua nafasi ya Tobias Hans wa CDU. Kiongozi wa SPD Lars Klingbeil amesema jimbo la Saarland lilikuwa mtihani wa kwanza kuangalia hali ya mambo, baada ya uchaguzi wa shirikisho. Klingbeil ameuelezea ushindi huo kama ''ushindi wa kushanganza''.

''Haya ni mafanikio makubwa aliyoyapata Anke Rehlinger na SPD huko Saarland. Tunaona leo katika uchaguzi kuwa tuko juu sana. Haya ni matokeo ya kazi ngumu ya kikanda ya SPD, ambayo baada ya miaka 23 imefanikiwa kuchukua nafasi ya CDU katika jimbo hilo,'' alifafanua Klinbeil.

Infografik Wahlergebnis Saarland Landtagswahl DE
Matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Saarland, Ujerumani

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD kimeingia katika bunge la majimbo, baada ya kupata asilimia 5.7 ya kura. Chama cha kiliberali FDP, na chama cha Kijani kinachotetea ulinzi wa mazingira havikupata asilimia 5 ya kura inayohitajika, hivyo kwa sasa havitowakilishwi katika bunge jipya.

AfD na CDU vyama vya upinzani

Chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto Die Linke, pia hakitakuwepo kwenye bunge la jimbo kutokana na kupata asilimia 2.6 ya kura, ikilinganishwa na uchaguzi wa mwisho miaka mitano iliyopita kilipojinyakulia asilimia 12.8 ya kura. Vyama vya AfD na CDU vitakuwa vyama pekee vya upinzani katika bunge hilo la jimbo.

Uchaguzi wa Saarland ni wa kwanza kati ya chaguzi tatu za mabunge ya majimbo zinazofanyika mwaka huu katika majimbo yanayoongozwa na mawaziri wakuu kutoka CDU. Uchaguzi muhimu zaidi utafanyika Mei 15, katika jimbo lenye wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani la North Rhine-Westpahalia. Jimbo jengine linaloongozwa na CDU ni Schleswig Holstein litakalopiga kura Mei 8. Jimbo la Lower Saxony ambalo kwa sasa linaongozwa na SPD, litapiga kura mwezi Oktoba.

(DPA, Reuters)