1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji nchini Israel walishambulia lori la msaada

Tatu Karema
17 Mei 2024

Mamia ya waandamanaji wa Israel leo wameshambulia lori moja katika eneo la ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu na kumpiga dereva wake kabla ya kuliteketeza.

https://p.dw.com/p/4g0hL
Malori ya misaada kwa ajili ya Gaza
Malori yaliyobeba misaada kuelekea GazaPicha: GIUSEPPE CACACE/AFP via Getty Images

Mamia ya waandamanaji wa Israel leo wameshambulia lori moja katika eneo la ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu na kumpiga dereva wake kabla ya kuliteketeza lori hilo katika jaribio la kuzuia msaada kufikishwa Ukanda wa Gaza. Haya yamesemwa leo na jeshi la Israel.

Jeshi hilo limesema maafisa wake walifika kwenye eneo hilo la tukio na kumuokoa dereva huyo pamoja na kumpa huduma ya matibabu.

Jeshi hilo limeongeza kuwa waandamanaji hao pia waliwashambulia wanajeshi wake na kuwajeruhi kidogo maafisa wawili.Israel yasema imeruhusu msaada zaidi kuingia Gaza

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa lori hilo lilikuwa limebeba bidhaa za kawaida za kibiashara na wala sio msaada kwa Gaza.

Hii leo, malori yaliokuwa yamebeba bidhaa za msaada zinazohitajika kwa wingi katika Ukanda wa Gaza, yalipitia gati la kuelea lililojengwa na Marekani kuingia katika eneo hilo lililozingirwa kwa mara ya kwanza wakati vizuizi vya Israeli vya kuvuka mipaka na mapigano makali yakizuia kufikishwa kwa chakula na bidhaa nyingine kwa watu katika eneo hilo.