1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaomba masoko ya wanyama hai kufungwa

Lilian Mtono
13 Aprili 2021

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa mwito wa kupiga marufuku uuzwaji wa wanyama hai kwenye masoko ya vyakula ili kuzuia kuzuka kwa maradhi mapya.

https://p.dw.com/p/3rviA
Schweiz | Tedros Adhanom Ghebreyesus - Direktor der WHO
Picha: Martial Trezzini/Keystone/picture alliance

Shirika hilo limesema baadhi ya visa vya COVID-19 vilivyogunduliwa awali vilikuwa na mahusiano na vyakula vilivyouzwa kwenye soko la jumla la vyakula kwenye mji wa Wuhan nchini China, na wagonjwa wengi wa mwanzoni walikuwa ni wamiliki wa maduka, wafanyakazi wa sokoni ama wanunuzi waliotembelea soko hilo.

Limesema "wanyama na hususan wa porini ni chanzo cha zaidi ya asilimia 70 ya magonjwa ya kuambukiza kwa binadamu, na mengi miongoni mwa magonjwa hayo yanasababishwa na virusi vipya ambavyo havijawahi kurekodiwa kabla. Wanyama wa porini, husababisha kitisho cha kuibua maradhi mapya".

WHO imesema ingawa masoko hayo yana mchango mkubwa kuanzia uuzwaji wa vyakula kwa idadi kubwa ya watu hadi kutengeneza kipato, lakini hatua hiyo ya kuzuia biashara ya wanyama hai inaweza ikasaidia kulinda afya za wauzaji na wanunuzi. Kulingana na WHO, tayari kumeandaliwa mwongozo wa muda kuhusiana na hatua hiyo kwa ushirikiano na shirika la kimataifa la afya ya wanyama, OIE pamoja na mpango wa kimataifa wa mazingira, UNEP.

"Masoko yanayouza wanyama hao, ambako pia huchinjwa na kuandaliwa pia yanaleta kitisho cha kusambaza virusi ama bakteria au wadudu wanaoweza kusababisha maradhi kwa wahudumu ama wanunuzi, umesema mwongozo huo wa OIE na UNEP.

WHO pia imetoa mwito kwa serikali kufunga maeneo yanayouza wanyamapori hai, hadi pale kutakapokuwa kumefanyika tathmini ya kutosha.

Tizama Video: 

Vidokezo kuhusu virusi vya Corona

Mashirika: AP