1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yazikosoa nchi tajiri kutoa chanjo ya tatu ya COVID-19

Grace Kabogo
19 Agosti 2021

Shirika la Afya Duniani, WHO limezikosoa nchi tajiri duniani kwa kuanza kutoa chanjo ya tatu ya nyongeza ya COVID-19, huku mamilioni ya watu katika nchi masikini wakiwa bado hawajapata hata dozi moja ya chanjo. 

https://p.dw.com/p/3zBCb
Covid-19 Impfstoff Johnson and Johnson
Picha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Wataalamu wa WHO wamesema hakuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi unaoonesha kwamba chanjo za nyongeza zinahitajika kwa watu ambao tayari wamechanjwa mara mbili, na iwapo hilo litafanikisha kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza siku ya Jumatano na waandishi habari mjini Geneva, Mkurugenzi wa masuala ya Dharura wa WHO, Mike Ryan amesema ukweli wa kimsingi na kimaadili ni kwamba wanataka kuwaokoa kwa mara ya pili watu, huku wakiwaacha mamilioni ya watu bila msaada wowote wa kuwalinda.

"Tunapanga kutoa jaketi zaidi za kuokolea maisha kwa watu ambao tayari wanazo, na tunawaacha watu wengine wazame, bila ya kuwa na jaketi ya kuokolea maisha hata moja. Huo ndiyo ukweli. Sayansi haina uhakika juu ya hili," alifafanua Ryan.

Schweiz Genf | Mike Ryan Stellvertretender Generaldirektor der WHO während Pressekonferenz
Mkurugenzi wa masuala ya Dharura wa WHO, Mike RyanPicha: picture-alliance/KEYSTONE/S. Di Nolfi

Kauli hiyo ameitoa muda mfupi kabla ya Marekani kutangaza kwamba Wamarekani wote waliopewa chanjo, watapokea dozi za ziada kuanzia Septemba 20. Chanjo hizo za nyongeza zitatolewa miezi minane baada ya mtu kuwa amechoma chanjo kamili.

Mapema mwezi Agosti, WHO ilitaka kusitishwa kwa utoaji wa chanjo za nyongeza za virusi vya corona ili kusaidia kupunguza ukosefu mkubwa wa usawa katika usambazaji wa dozi kati ya mataifa tajiri na masikini.

Hata hivyo, hilo halijazuia nchi kadhaa kuendelea na mipango yao ya kuongeza chanjo ya tatu ya nyongeza, zikiwa zinaendelea kujitahidi kupambana na kirusi cha corona aina ya Delta.

Wamarekani kulindwa

Mkurugenzi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani, CDC, Rochelle Walensky amesema mpango wao ni kuwalinda watu wa Marekani na kukishinda kirusi hicho.

Israel tayari imeanza kutoa chanjo za tatu kwa raia wote wa nchi hiyo wenye umri wa miaka 50 na juu ya hapo.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kilicho wazi ni kwamba kuna umuhimu wa kupata dozi za kwanza na kuwalinda watu walioko hatarini zaidi, kabla ya kuanza kutoa chanjo za nyongeza.

Soma zaidi: WHO yazilaumu nchi tajiri kujilimbikizia chanjo za COVID-19

Ghebreyesus amesema mgawanyiko uliopo kati ya walionacho na wasionacho utaongezeka zaidi iwapo kampuni za madawa za kutengeneza chanjo pamoja na viongozi watatoa kipaumbele katika utolewaji wa chanjo za nyongeza, kuliko usambazaji wa chanjo za kwanza kwa nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

WHO - Ebola-Lage im Kongo | Matshidiso Moeti
Mkurugenzi wa WHO Afrika, Matshidiso Moeti Picha: picture-alliance/dpa/KEYSTONE/S. Di Nolfi

Kwa upande wake mkurugenzi wa WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti ameukosoa vikali uamuazi wa baadhi ya nchi tajiri kuanza kutoa chanjo za nyongeza za virusi vya corona.

Akizungumza siku ya Alhamisi na waandishi habari, Moeti amesema maamuzi hayo yanatishia ahadi ya mustakabali wa Afrika iliyo bora.

Kwa mujibu wa maafisa wa afya barani Afrika, hadi sasa chini ya asilimia mbili ya watu wa bara hilo lenye jumla ya watu bilioni 1.3 ndiyo wamepata chanjo kamili ya COVID-19.

 

(AFP, AP, DW https://bit.ly/2VZMILb)